Njia tano za kipekee walizotumia Waafrika kuhifadhi chakula kabla ya ujio wa majokofu

Chakula ni jambo la lazima kwa binadamu. Uhifadhi wa chakula kabla ya ujio wa majokufu katika karne ya 18, ulihusisha mbinu za asili. Katika nchi za Ulaya zenye baridi kali, mapande ya barafu na masanduki ya barafu yalitumika kwa miaka mingi kuhifadhi chakula.
Barani Afrika, ambako sehemu kubwa ni eneo la jua, kulikuwa na mbinu vilevile za kiasili za kuhifadhi chakula ili kikaae muda mrefu bila kuharibika, kwa matumizi ya baadaye.
Turudi nyuma kwanza: Mchakato wa kuunda majokofu ya kisasa ulitokana na kazi ya wavumbuzi kadhaa katika miaka ya 1800 katika mataifa ya Marekani na Ujerumani. Uvumbuzi huo ulisababisha kuenea kwa majokofu ya kibiashara mwanzoni mwa karne ya 20 katika maeneo ya viwanda vya kutengeneza pombe na viwanda vya nyama.
Mwaka 1913, Mmarekani Fred W. Wolf alivumbua jokofu la kwanza la umeme la nyumbani. Na hatiyame, uzalishaji mkubwa wa majokofu ulianza mwaka 1918.
Jokofu ni kifaa cha umeme ambacho huhifadhi chakula kwa kutumia baridi ili kuzuia kisiriharibike. Hufanya kazi kwa kutumia umeme kupoza ndani ya hokofu hadi halijoto la chini.
Kabla ya ujio wa majokofu barani Afrika, watu wamehifadhi chakula kwa maelfu ya miaka, na hata katika miaka hii, maeneo ambayo huduma ya umeme haijafika au uwezo wa kumiliki jokofu ni mdogo, bado njia hizi za asili zinatumika.
Kutumia chumvi

CHANZO CHA PICHA, MAKEFOODSTAY
Chumvi imetumika kuhifadhi chakula kwa karne nyingi. Chumvi hutumiwa kwa njia mbili za kuhifadhi vyakula, chumvi ya madonge au maji ya chumvi. Barani Afrikam, chumvi ilikuwa muhimu katika kuhifadhi chakula majumbani na wakati wa safari.
Mtafiti wa biolojia na dawa kutoka Chuo Kikuu cha Carlifornia, Berkey, Dr. Ingrid Koo, anasema chumvi hupunguza molekuli za maji katika chakula na viumbe vyote vilivyo hai vinahitaji maji. Kwa sababu hiyo haviwezi kukua bila maji – ikijumuisha bakteria wanaoweza kusababisha sumu kwenye chakula na kuharibika.
Huu ni mchakato wa chumvi kuondoa molukule za maji na kuweka molukule za chumvi katika chakula. Vilevile, chumvi ikiwa nyingi huwa sumu kwa baadhi ya vijidudu.
Nyama ya ng’ombe na samaki, ni mifano michache tu ya vyakula ambavyo huhifadhiwa kwa kutumia chumvi. Ni kweli inaweza kuviweka salama vyakula kwa muda mrefu, lakini haiondoi kabisa uwezekano wa kuharibika.
Kutumia moto

CHANZO CHA PICHA, PJP
Bakteria na kuvu husababisha kuharibika kwa chakula na kuleta magonjwa yanayotokana na chakula. Moto umetumika kuhifadhi chakula kupitia kuoka, kuchoma, kukausha, na kukipika. Aina zote hizo ni mbinu za kizamani za kupunguza nguvu ya wadudu kuharibu chakula.
Kukipika chakula kutokana na moto huuwa vjijidudu na kuzuia ukuaji wake. Kuchoma, kuoka au kukausha chakula hupunguza maji ya chakula na kuua vijidudu, ambavyo vinaweza kuingia katika chakula wakati wa mavuno, uchinjaji, usafirishaji na mazingira mengine.
Fauka ya hayo, moto huongeza pia ladha ya chakula kinapopikwa. Nyama iliyopikwa au kuchomwa, ladha yake haiwi sawa na nyama mbichi uitiapo mdomoni. Mfano huu ni kwa vyakula vyote ambavyo vinahitaji kupikwa kabla ya kuliwa.
Kukausha na Jua

CHANZO CHA PICHA, BBURI
Mbinu ya zamani kabisa ya kuhifadhi chakula ni kupunguza maji katika chakula kwa kutumia jua. Vyakula viliwekwa katika jua kali na kukaushwa, mfano; matunda, mboga mboga, na nyama. Njia hii inahusisha kuweka chakula kwenye jua moja kwa moja ili kuyeyusha unyevu na kuzuia ukuaji wa bakteria ili kuzuia kuharibika.
Ili kufanikiwa, inahitaji msimu usio na mvua. Mchakato huu ni sawa na ule wa matumizi ya moto, kwani bakteria wengi huhitaji unyevu kukua na kuishi. Kwa kukausha chakula, unapunguza kwa kiasi kikubwa maji, na kukifanya chakula kuwa ni mazingira yasiyorafiki kwa vijidudu.
Katika nchi zenye jua kali barani Afrika, njia hii ya kale ya kujifadhi chakula, haikuhitaji uwepo wa viwanda vikubwa vya kusindika vyakula au kugandisha chakula katika majokofu ya kisasa.
Kufukia kwenye udongo

CHANZO CHA PICHA, EOS
Udongo uko kila sehemu. Binadamu hutegemea udongo kwa asilimia 95 kwa ajili ya kupata chakula, iwe mazao tunayokula, au mboga na mimea mingine ili kulisha wanyama kwa ajili ya nyama. Na hiyo ni sehemu moja tu ya faida ya udongo.
Udongo umetumika kuhifadhi chakula kwa kukizika, hasa vyakula vya mizizi kama muhogo ili visiharibike. Njia hii pia imetumika kuhifadhi mboga zenye mizizi na baadhi ya matunda, ili kutoa ulinzi.
Kufukia chakula kunatoa ulinzi dhidi ya mwanga au joto au hali ya hewa ya baridi. Mbinu hii pia inaweza kufanya kwa kushirikiana na mbinu nyingine za kuhifadhi chakula kama kutia chumvi.
Kutumia Barafu

CHANZO CHA PICHA, LONDONDAILY
Licha ya kuwa sehemu kubwa ya bara la Afrika haina misimu ya theluti. Njia ya kutumia barafu kuhifadhi chakula imetumika kwa karne nyingi, hasa katika maeneo ambayo misimu ya baridi ni mirefu na jua hukosekana.
Kwa hakika njia hii, ndio ilibadilishwa kutoka kutumia masanduku yenye barafu za kawaida, hadi kutumia majokufu ambayo huzalisha hali ya hewa ya baridi na mapande ya barafu kwa ajili ya kuhifadhi kila aina ya chakula, katika nchi masikini na zile tajiri.
Barafu hutumiwa kuhifadhi chakula kwa kupunguza kasi au kuzuia ukuaji wa vijidudu vinavyosababisha kuharibika chakula. Mbinu hii ilihusisha kuchimba maeneo yenye barufi na kuweka chakula au kuweka chakula kwenye masanduku ya mbao au chuma yaliyojazwa mapande ya mabarafu.