Papa ajaye atakuwa na asili ya Afrika?

Mchakato wa kuanza kumtafuta Papa mpya umeaanza rasmi Mei,07, 2025. Kiongozi huyo wa Kanisa Katoliki duniani atakuwa Papa wa 267 kufuatia kifo cha Papa Francis Mwezi uliopita.
Kama ukuaji wa Kanisa Katoliki ungelikuwa ndio kipimo pekee cha kutabiri mahali ambapo Papa ajaye atatokea, basi ishara zote zingeelekeza Afrika kama chimbuko lake jipya.
Barani Afrika, imani ya Kikatoliki inachanua kwa kasi ya kipekee ikiongezeka kwa asilimia 3.31% kati ya mwaka 2022 na 2023.
Takwimu mpya kutoka Vatican zinaonesha kuwa sasa, mmoja kati ya Wakatoliki watano duniani anaishi Afrika.
Kwa upande mwingine, Ulaya ambayo kwa karne nyingi imekuwa kitovu cha Ukristo inashuhudia kudorora kwa imani hiyo.
Katika kipindi hicho hicho cha miaka miwili, ukuaji wa Wakatoliki ulikuwa wa polepole mno, kwa asilimia 0.2% tu.
Tangu mwaka 1910 hadi 2010, idadi ya Wakatoliki barani Ulaya imepungua kwa zaidi ya asilimia 63, kulingana na utafiti wa Kituo cha Pew kilicho Marekani.
Ulaya sasa inaelezwa kuwa miongoni mwa jamii zinazopendelea maisha ambayo hayafungamani na dini ukilinganisha na hapo awali.
Katika Amerika ya Kusini, ingawa Kanisa Katoliki bado lina ushawishi mkubwa, linapoteza ufuasi wake kwa kasi mbele ya madhehebu ya Kipentekoste.
Utafiti wa mwaka 2022 kutoka Latinobarómetro katika nchi 18 za eneo hilo unaonesha kupungua kwa wale wanaojitambulisha kama Wakatoliki kutoka asilimia 70 mwaka 2010 hadi asilimia 57 mwaka 2020.

CHANZO CHA PICHA, GETTY IMAGES
Hivyo basi, wakati makadinali watakaopiga kura watakapokutana mjini Vatican kumchagua mrithi wa Papa Francis, je, asili ya mgombea inapaswa kuwa miongoni mwa vigezo vya uamuzi wao?
Padri Stan Chu Ilo, raia wa Nigeria na profesa mwandamizi katika Chuo Kikuu cha DePaul, anaamini kuwa jambo hilo halipaswi kupuuzwa.
“Nadhani ingekuwa hatua ya kihistoria na ya kutia moyo kumpata Papa kutoka Afrika,” anasema, akisisitiza kuwa uongozi wa Kanisa unapaswa kuakisi sura halisi ya waumini wake kote duniani.
Papa Francis, tangu kuchaguliwa kwake mwaka 2013, ameongeza uwakilishi wa makadinali kutoka Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara katika kundi la wapiga kura wa Papa mpya – kutoka asilimia 9 hadi asilimia 12 kufikia mwaka 2022.
Hata hivyo, kwa mujibu wa Padri Chu Ilo, ongezeko hilo pekee halitoshi kama halitaambatana na nia ya dhati ya kuwachagua viongozi kutoka bara la Afrika.
Anaeleza kuwa mara nyingi makadinali hupendelea kuchagua mgombea mwenye hadhi ya juu na umaarufu kimataifa: “Mtu ambaye tayari ni sauti yenye ushawishi mkubwa ndani na nje ya Kanisa.”
Changamoto kubwa, anasema, ni ukosefu wa viongozi wa juu wa Kiafrika katika nafasi muhimu ndani ya Vatican kwa sasa. “Ukitazama orodha ya makadinali wa Kiafrika wanaotajwa kuwa na nafasi ya kupanda hadhi kuwa Papa, ni nani kwa kweli anayeng’ara katika majukwaa ya Katoliki ya kimataifa kwa sasa? Ukweli wa kusikitisha ni kwamba hakuna.”

CHANZO CHA PICHA, GETTY IMAGES
Hili, analosema Padri Chu Ilo, linatofautiana sana na hali ya mwaka 2013, ambapo Kadinali Peter Turkson kutoka Ghana alikuwa miongoni mwa wagombea waliokuwa na nafasi kubwa ya kuchaguliwa kuwa Papa.
Vilevile, mwaka 2005, Kadinali Francis Arinze kutoka Nigeria alitajwa kama mgombea mwenye uwezekano mkubwa katika mkutano wa makadinali uliomchagua Papa Benedikto wa XVI.
“Jinsi tulivyofikia hali hii kwa bara la Afrika na Kanisa Katoliki bado ni jambo linalowashangaza wengi wetu, hasa ikizingatiwa mtazamo wa wazi wa Papa Francis kuhusu Afrika,” anasema Padre Chu Ilo.
‘Kidokezo cha kuhongwa’
Ingawa historia inatambua kuwepo kwa Mapapa watatu kutoka Afrika, wa mwisho Papa Gelasius wa Kwanza aliyefariki zaidi ya miaka 1,500 iliyopita.
Kwa mtazamo wa wengi, huu ni wakati muafaka kwa Papa mwingine kutoka Afrika.
Hata hivyo, baadhi ya Wakatoliki wa Kiafrika wanaamini kuwa mjadala wa Papa ajaye unatilia mkazo kupita kiasi juu ya asili yake ya kijiografia.
Miongoni mwao ni Padri Paulinus Ikechukwu Odozor, profesa katika Chuo Kikuu cha Notre Dame na padri wa Kanisa Katoliki aliyezaliwa Nigeria.
“Sijawahi kuamini kuwa kwa sababu umetoka Afrika au Ulaya basi unastahili kuwa Papa,” anasema.
“Mahali unapotoka si jambo la msingi. Mara tu unapochaguliwa, masuala ya waamini wote yanakuwa yako. Lengo lako kuu linapaswa kuwa kujenga mwili wa Kristo bila kujali watu wako wapi, wako wangapi, au wanakabiliwa na mazingira gani.”
Anasisitiza kuwa jambo la msingi zaidi ni kwamba Papa awe “mtaalamu mkuu wa elimu ya dini.”
Kwa mujibu wake, Papa anapaswa kuwa mtu anayefahamu kwa undani tamaduni za Kanisa, na awe na uwezo wa kutumia maarifa hayo kuwaongoza waumini kwa hekima na mwelekeo sahihi.

CHANZO CHA PICHA, GETTY IMAGES
Padri Odozor anasema hukatishwa tamaa kila anapoulizwa iwapo Papa ajaye anapaswa kutoka Afrika, akieleza kuwa swali hilo linabeba taswira ya kupewa nafasi kwa ajili ya idadi tu, badala ya sifa na uwezo.
“Ni kana kwamba watu wanasema, ‘Kwa kuwa Waafrika sasa ni wengi ndani ya Kanisa, basi tuwape Papa wao.'”
Kwa mtazamo wake, kuna haja ya mabadiliko ya kweli ili kuhakikisha kuwa masuala yanayowahusu waumini wa Katoliki barani Afrika yanapewa uzito unaostahili na viongozi wa ngazi za juu ndani ya Vatikan.
Anasema kwamba wakati mwingine hali hiyo huashiria kana kwamba Waafrika hawazingatiwi, au imani yao haionekani kuwa ya kiwango cha juu, bali ni duni au bandia, na hivyo haifai kuchukuliwa kwa uzito.
“Waafrika wanapohisi kuwa masuala yao hayawekwi mezani kama yanavyopaswa, ndipo watu huanza kujiuliza: labda njia pekee ya kusikilizwa au kuonekana ni kuwa na mtu wetu kule hasa wadhifa wa Papa.”
Ubaguzi wa rangi kanisani?
Padri Chu Ilo, naye anahisi kwamba licha ya kuongezeka kwa idadi ya makadinali kutoka bara la Afrika, bado hawana mamlaka halisi ndani ya Kanisa.
“Sikatai ubora wa makadinali wanaoteuliwa na Papa Francis,” anaeleza.
Lakini anauliza, “Unapowateua, je, unawapa mamlaka? Wape hawa watu unaowateua uwezo, waamini na uwape fursa ya kutekeleza majukumu yao.”
Padri Chu Ilo na Padri Odozor wote wanaangazia tatizo moja linaloweza kudhoofisha jitihada za Papa Francis za kufanya uongozi wa Kanisa kuwa na uwakilishi zaidi.
“Bado kuna swali la ubaguzi wa rangi ndani ya Kanisa ambalo hatujawahi kulizungumzia,” anasema Padri Odozor.
“Tatizo hili linaweza kumdhoofisha mtu yeyote, hata awe na sifa za Kipapa kiasi gani au afanye kazi gani; atachukuliwa tu kama Papa wa Kiafrika.”
Mwisho wa mwaka 2022, Papa Francis alikuwa amewateua karibu theluthi mbili ya makadinali watakaomchagua mrithi wake idadi inayokaribia wingi wa kura zinazohitajika kumchagua Papa mpya.
Hii ina maana kwamba yeyote atakayechaguliwa, kuna uwezekano mkubwa atashikilia msimamo wa Papa Francis wa kuwaleta karibu maskini na waliotengwa.
Huu ni mtazamo ambao Padri Chu Ilo anauita “mtazamo wa maskini kwanza,” ukiwa na lengo la kuwa “Kanisa linalosikiliza, Kanisa lenye maadili ya kisasa, na Kanisa lenye unyenyekevu.”
Hicho ndicho anachotamani kukiona kwa yeyote atakayekuwa kiongozi wa Kanisa katika siku zijazo.

CHANZO CHA PICHA, GETTY IMAGES
Uwezekano wa kustaajabu
Lakini kuna kipengele kingine muhimu kinachofanya kuwa vigumu kutabiri ni nani atakayechaguliwa, anasema Padre Chu Ilo.
“Wakristo wa Katoliki wanaamini kwamba Mungu, kupitia Roho Mtakatifu, husaidia katika kuchagua viongozi wa Kanisa,” ananieleza.
Hii inamaanisha kwamba matokeo yanaweza kuwa ya kushangaza, kama ilivyotokea mwaka 2013 wakati Papa Francis alichaguliwa. “Hakuwa yule aliyetabiriwa na mtu yeyote,” anasema Padre Chu Ilo.
Ninamuuliza, anadhani nini ni muhimu zaidi kwamba Papa atakayefuata aendelee na maono ya mtangulizi wake kwa ajili ya Kanisa, au kwamba awe kutoka Afrika?
“Nitajibu kama kasisi mwenye busara,” ananijibu akicheka.
“Nitamwomba Mungu atujaalie Papa atakayekuza mtazamo wa Francis, na nitaomba kwamba mtu wa aina hiyo atoke Afrika.”