Kutembea pekupeku kunavyoweza kukuokoa na kifo

Ni saa mbili asubuhi katika eneo la Kasarani, kaunti ya Nairobi nchini Kenya…Ninakutana na daktari wa masuala ya afya ya binadamu Hamisi Kote Ali akijiandaa kuanza kazi yake, kinachonivutia macho ni kutovaa viatu, Naam anatembea miguu peku.
Ni mwaka wa sita sasa tangu aamue kutembea bila viatu, nilipomuuliza iwapo ni viatu amevisahau kuvaa.
”Niliamua kutembea miguu chuma miaka 6 iliyopita nilipofanya utafiti wangu wa kina nilipokuwa mafunzoni Marekani kuhusu ufanisi wa wanariadha wa Kenya haswa wanapokimbia bila viatu, Daktari Hamisi alinieleza.
Na sio hapa nchini Kenya anatembea bila viatu amesafiri mataifa ya ughaibuni bila viatu.
”Nimeenda Ufaransa, Italia na pia mwaka jana Disemba nilikuwa Uarabuni, katika safari yangu yote hadi kuabiri ndege nilikuwa miguu peku”, aliniambia
Kuna wanawake na wanaume wengi wananunua viatu ghali nakujipata wanatembea kama bata,” kununua viatu ni kununua ugonjwa, kwasasa hutaona madhara yake lakini fainali ni uzeeni” Dkt Hamis ananieleza.
Wengi huchukulia kutembea bila viatu kama ishara ya umaskini na uzembe lakini je kuna kitu cha maana zaidi katika kutembea miguu peku ?
Umuhimu wa kutembea pekupeku
Katika ulimwengu wa kisasa, mara nyingi tunatumia muda mwingi tukiwa tumevaa viatu, tukiwa ndani ya nyumba, maofisini, au mitaani.
Hata hivyo, kutembea bila viatu, ni tabia yenye manufaa mengi kiafya ambayo imekuwa ikisahaulika.
”Jointi za miguu ni 33 na ni sawia na jointi za kiunoni 33 hadi shingoni na kila unapokanyaga unafanya viungo vijiachilie”, kwa mujibu wa dkt Hamisi .
Kisha anaendelea kutueleza, ”Unapovaa viatu vidole vya miguu hubanika na inaathiri jointi za kiunoni na hapo changamoto za afya huanza kujitokeza, Hamisi anasema.
Japokuwa karne ya 21 kila mmoja anahangaika na wengine kugharamika kununua viatu, faida ya kuvaa viatu ni mbili, haya ni kwa mujibu wa daktari wa mifupa Hamisi Ali Kote.
”Ukivaa viatu unafaida mbili ni urembo na pia hukuzuia kupata majeraha.”
Ushahidi wa kisayansi kuhusu kutembea pekupeku
Kwa mujibu wa utafiti ambao daktari kote amegundua ni kuwa kugusa ardhi moja kwa moja kwa ngozi ya miguu husaidia kusawazisha chaji ya umeme mwilini, hali inayojulikana kama ”earthing” au ”grounding” hili linaweza kupunguza mfadhaiko wa akili, kuimarisha usingizi na kupunguza maumivu sugu mwilini.
Baadhi ya magonjwa unayoweza kutibu kupitia kutembea pekupeku ni kama vile:
- Kisukari
- Shinikizo la damu
- Hasira
- Ukosefu wa kinga mwilini
Kama ni tiba kama wataalam wanavyosema, maana yake inaweza kukuokoa na kifo ambacho kingetokana na magonjwa haya.
Lakini si tu faida za kimwili zinazopatikana kuna jambo la kihisia na kiroho. Kutembea peku huchochea hisia kuunganishwa na dunia.
”Mimi hutembea miguu peku pia kama nafasi yangu ya kiroho hasa kuwa rafiki wa udongo kwani binadamu tuliumbwa kwa udongo na hapo ndipo tutakaporudi”
Bila shaka dunia ya leo ina changamoto zake si kila mahali ni salama kutembea miguu peku. Nilipenda kujua ameepukaje kupata majeraha tangu aanze mtindo huu wa maisha.
”Unapotembea bila viatu unamakinika zaidi kutokana na nyayo zako kugusa ardhi kinyume na ukiwa umevaa viatu, waliovaa viatu mara nyingi wanatembea barabarani na hawapo walipo kwahivyo ni vigumu kwangu kukunguwaa, dkt Hamisi Kote anasema.
”Unyanyapaa bado upo”
Katika enzi hizi za kisasa ambapo teknolojia na mitindo ya maisha vinachukua nafasi kubwa katika jamii, kunao waliomwita mwendawazimu na aliyekuwa na msongo wa mawazo wanapomuona akitembea miguu peku mitaani.
”Nilipoanza kutembea bila viatu watu hasa jamii yangu ya karibu walinifikiria napitia mazito maishani, nina kasoro wengine wakinikejeli mke wangu ataniacha,” anasema Dkt Hamisi kote.
Dk. Hamisi, mtaalamu na mwanzilishi wa Kikundi cha Ustawi wa Garage ya Binadamu, alishauri watu kutembea bila viatu angalau nusu saa kwa siku kunaweza kuwa na athari chanya kwa afya.
Chaguo lake la maisha lisilo la kawaida limezua mijadala, huku wengi wakivutiwa na wazo la kuweka msingi na manufaa yake ya kiafya.
Mrisho Mpoto, msanii wa Tanzania

CHANZO CHA PICHA, MPOTO
Na sio tu Kenya pia nchi jirani ya Tanzania, msanii Mrisho mpoto pia amekiri kutovipa umuhimu viatu maishani mwake.
Kupitia mahojiano aliyowahi kufanya na vyombo vya habari Tanzania anasema anafuata mababu wa jadi ambao hawakuvaa viatu na pia anachota madini kutoka ardhini.
”Waswahili wanasema ardhi imemeza vingi kwa maana hiyo unavyotembea bila viatu unachota vilivyomo, nachota maarifa kupitia kutembea miguu peku” anasema Mrisho Mpoto.
Wengine wanaotembea pekupeku

Katika ulimwengu wa sanaa na ubunifu, kuna kundi la wasanii mashuhuri waliamua kuacha kiatu si kwa sababu ya uhitaji bali kwa sababu ya msukumo wa ndani, falsafa, au uhalisia wa maisha yao.
Miongoni mwao ni kama vile:
1.Benjamin Clementine
Muingereza mweusi, mshairi mahiri, mwimbaji mwenye sauti ya kipekee, mtunzi, na mcheza vyombo vya muziki.
Alipopanda jukwaani na piano, viatu vilimkosesha uhuru wa kugusa pedali kwa ufasaha.
Hapo ndipo alipofanya uamuzi wa kipekee kuvivua viatu na kuruhusu miguu yake iguse uhuru wa uhalisia wa muziki.
Tangu wakati huo, safari yake na viatu ilifikia kikomo.
2. Allan Mutabaruka
Kutoka Jamaica, tunamwona Allan Mutabaruka, mwanamuziki, mwigizaji, mwalimu, na mtangazaji wa vipindi vya mazungumzo, ambaye maisha yake peku yamekuwa alama ya msimamo wa kiutamaduni na kijamii.
Utambulisho wake unakwenda sambamba na ardhi miguu yake haiogopi vumbi wala baridi.
3. Wanlov Kubolor
Kule Ghana, jina la Wanlov the Kubolor linang’aa si tu kwa muziki wake wa kipekee bali pia kwa mtazamo wake wa maisha.
Kwake, kutembea peku si mtindo, ni mawasiliano lugha ya mwili na ardhi.
Anasema, ardhi ina kumbukumbu, na kupitia miguu yake isiyo na vizuizi, anakumbuka hisia za kila mahali alipopita.
Ni mawasiliano ya kimya kati ya msanii na dunia yake.
4. Cesária Évora
Tunasafiri hadi Cape Verde na kumpata Cesária Évora, “Malkia wa Morna”, aliyejizolea sifa na heshima ulimwenguni kote.
Ingawa sasa ni marehemu, urithi wake wa kutembea peku majukwaani uliwasilisha ujumbe wa uhalisia na ujivuni wa chimbuko lake.
Akiwa mtoto, viatu vilikuwa nadra kwake, na alipopevuka, alikumbatia hali hiyo kama alama ya maisha halisi na uhuru wake wa kisanii.
5. Michael Franti
Na hatimaye, tunakutana na Michael Franti kutoka Marekani.
Safari yake ya peku ilianza baada ya kushuhudia watoto wasio na viatu katika pembe mbalimbali za dunia.
Akaona, badala ya kuzungumza tu, avue viatu na kuwa sauti ya kimya inayoonekana akilaani ukosefu wa haki na kuonyesha mshikamano.
”Katika dunia inayoendelea kujitenga na asili, kuna sauti za watu wachache wanaotufundisha kwamba labda, hatua ya kwanza kuelekea afya bora, ni kuikanyaga dunia… miguu peku”, nukuu ya mfuatiliaji wa mtindo huu katika mtandao ya kijamii.