Leo XIV kutoka Marekani ndiye Papa mpya

Kadinali Robert Prevost ametangazwa kuwa Papa mpya.
Papa Robert Prevost atajulikana kama Papa Leo XIV.
Prevost ni mzaliwa wa Chicago nchini Marekani, na hadi kuchaguliwa kwake alikuwa akihudumu kama mkuu wa Dicastery wa kanisa kwa Maaskofu.
Papa Leo XIV mwenye umri wa miaka 69 ametumia muda wake mwingi akitumikia nchini Peru, na ana uraia wa Marekani na Peru.

CHANZO CHA PICHA, REUTERS
Akihutubia umati uliokuwa ukishangilia kwa Kiitaliano, Papa Leo XIV alisema: “Amani iwe nanyi nyote.
“Wapenda, ndugu na kina dada, hii ni salamu ya kwanza ya ufufuko wa Kristo. Ningependa kutoa salamu ya amani iwafikie familia zenu, ninyi nyote, popote mlipo. Amani iwe nanyi.”
Alitoa shukrani kwa mtangulizi wake, Papa Francis, huku akisema anataka kuwasilisha baraka zake kwa watu kama Papa Francis alivyofanya mara ya mwisho alipojitokeza katika uwanja wa St Peter’s Square.
“Ubinadamu unahitaji Kristo kama daraja la kufikiwa na Mungu na upendo wake. Tusaidie, na tusaidiane, kujenga madaraja.”
Papa Leo XIV kisha aliwashukuru makadinali waliomchagua wakati wa mkutano wa siku mbili.
“Sote tunaweza kutembea pamoja kuelekea nyumba ya Mungu ambayo ametuandalia,” alisema. “Salamu maalum kwa Kanisa la Roma.”
Kisha papa Leo XIV alianza kuzungumza kwa Kihispania ili kushukuru dayosisi yake ya zamani huko Peru “ambapo watu waaminifu walishiriki naye imani na kujitolea kwa mengi”.
Leo XIV ahitimisha hotuba ya kwanza kama Papa

CHANZO CHA PICHA, REUTERS
Akirejelea kuzungumza Kiitaliano, papa mpya alitoa wito kwa umati wa watu kusali kwa Bikira Maria “pamoja” kwa ajili ya baraka zake.
Kisha akawaongoza watu katika sala ya haraka, ambayo ilipokelewa kwa shangwe.
Baada ya kuhitimisha hotuba yake, Papa mpya alianza kusoma kifungu cha kidini katika Kilatini akitoa heshima kwa watakatifu na Madonna.
Alipohitimisha hotuba yake kwa baraka zaidi, Papa Leo XIV alipungia mkono umati ambao ulikuwa umejaa katika sehemu kubwa ya Uwanja wa St Peter.

CHANZO CHA PICHA, GETTY IMAGES
Kabla ya kutangazwa, majina kadhaa yalikuwa yametajwa kumrithi Papa Francis kuongoza Kanisa Katoliki.
Baadhi ya majina hayo ni Kardinali Pietro Parolin alikuwa katibu wa mambo ya nje wa Vatican chini ya Papa Francis, na kumfanya kuwa mshauri mkuu wa Papa.
Peter Kodwo Appiah Turkson, Mganda wa kwanza kuteuliwa kuwa kardinali chini ya Papa John Paul II mwaka 2003, alipewa nafasi kubwa na watunga vitabu vya bahati nasibu kabla ya kupiga kura mwaka 2013 ambapo Francis alichaguliwa badala yake.
Kardinali Fridolin Ambongo Besungu anatoka Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC), ambako amekuwa Askofu Mkuu wa Kinshasa kwa miaka saba.
Kardinali Luis Antonio Gokim Tagle alitajwa kama chaguo muhimu. Kanisa Katoliki lina ushawishi mkubwa katika nchi yake ya Ufilipino, ambako takriban 80% ya watu ni Wakatoliki.
Makardinali Robert Prevost na Joseph Tobin, pia walitajwa mara kadhaa kama wanaowezekana kuwa warithi.
Mkutano wa siri wa kumchagua Papa ulianza jana katika kanisa la Sistine ukijumuisha makadinali 133 kutoka maeneo mbalimbali duniani.
Kuchaguliwa kwa Papa huyu kunafuatia kifo cha Papa Francis, aliyefariki akiwa na umri wa miaka 88 siku ya Jumatatu ya Pasaka 21 April, na mazishi yake kufanyika siku ya Jumamosi 26 April.
Huu ni mkutano wa tatu wa uchaguzi wa Papa unafanyika kwa siku mbili na kumpata Papa. Mikutano mingine ni ile iliyofanyika mwaka 2005 na 2013, ambayo ilidumu kwa siku mbili tu.
