Waafrika watatu wanaotajwa katika uchaguzi wa Papa

Waafrika watatu wanaotajwa katika uchaguzi wa Papa

Kongamano ambalo limepigiwa kura na Makadinali wa Kanisa Katoliki kumchagua Papa mpya, limeanza vikao tarehe 7 Mei. Vikao vya faragha vitafanyika katika Kanisa la Sistine na Makadinali 135 wanaruhusiwa kuhudhuria.

Haijulikani itachukua muda gani kumchagua Papa, lakini mikutano miwili ya awali iliyofanyika mwaka 2005 na 2013, ilidumu kwa siku mbili pekee.

Papa Francis alifariki Aprili 21 akiwa na umri wa miaka 88. Mazishi yake yalifanyika Jumamosi, Aprili 26. Msemaji wa Vatican, Matteo Bruni, alisema tarehe 7 Mei, Makardinali watashiriki Ibada ya Misa Takatifu katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Petro, ambapo wapiga kura watakusanyika katika Kanisa la Sistine kwa ajili ya vikao.

Wakiwa ndani ya kanisa la Sistine, Makadinali hawatakiwi kuwasiliana na ulimwengu wa nje hadi Papa mpya atakapochaguliwa.

Kuna duru moja tu ya upigaji kura siku ya kwanza katika majira ya alasiri. Kuanzia siku ya pili na kuendelea, Makadinali hupiga kura mara mbili kila asubuhi na mara mbili kila alasiri katika kanisa.

Ili kuchaguliwa kuwa Papa, mgombea lazima apate thuluthi mbili ya kura za wapiga kura Makardinali.

Wakati wa kupiga kura, kila mpiga kura huandika jina la mgombea anayempendelea kwenye karatasi ya kura chini ya maneno “Ninamchagua kama Papa Mkuu.”

Ili kuhifadhi usiri wa kura, Makadinali huagizwa kutotumia mwandiko wao wa kawaida. Iwapo hakuna kura ya uamuzi kufikia mwisho wa siku ya pili, siku ya tatu inatolewa kwa sala na kutafakari, bila kura yoyote kufanyika. Upigaji kura unaendelea kama kawaida baada ya siku hiyo.

Mchakato wote unaweza kuchukua siku kadhaa au hata wiki.

Mara mbili kwa siku, kura huchomwa, na watu walio nje ya Vatikani huona moshi ukitoka kwenye bomba la Kanisa la Sistine.

Wino mweusi au mweupe huwekwa kwenye kura. Moshi mweusi unamaanisha kura bado haijaamua. Moshi mweupe unaonyesha Papa amepatikana.

Makardinali watapigia kura wagombea hadi jina moja litokee. Huku asilimia 80 ya Makadinali wakiteuliwa na Papa Francis, hii ni mara yao ya kwanza kumchagua Papa – na watafanya hivyo kwa mtazamo mpana wa kimataifa.

Kwa mara ya kwanza katika historia, chini ya nusu ya Makadinali wapiga kura ndio wanatokea Ulaya. Brazil ina wawakilishi saba katika kundi hili.

Makadinali kutoka Afrika

Ni vigumu kutabiri nani atakuwa Papa. Kuna majina mengi yanayopendekezwa. Kutoka bara la Afrika, kuna majina matatu ambayo yako katika orodha.

Miongoni mwa Makadinali wanaotajwa; Kadinali Fridolin Ambongo Besengu wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo, Kadinali Robert Sarah kutoka Guinea na Kadinali Peter Turkson wa Ghana.

Fridolin Ambongo Besungu – Congo

fc

CHANZO CHA PICHA, FRANÇOIS-RÉGIS SALEFRAN –

Maelezo ya picha, Kadinali Fridolin Ambongo Besungu kutoka DR Congo

Besengu, ni Askofu mkuu wa Kinshasa, aliteuliwa na Francis mwaka 2019. Kwa sasa ana umri wa miaka 65, anaweza kutazamwa kama mdogo sana kuwa Papa. Kwa kawaida, Makadinali hawapendi kumchagua mtu mdogo, kwani inaweza kuwa na athari ya muda mrefu kwenye siasa na kanisa.

Akiwa Askofu katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo, Besengu alisimama kumkosoa Rais Joseph Kabila baada juhudi zake za kupeleka mbele uchaguzi, jambo ambalo linaashiria nia yake ya kukosoa viongozi wa kiimla.

Anapinga sana mapenzi ya jinsia moja. Wakati Francis alipotoa ruhusa ya baraka kwa watu wa mapenzi jinsia moja, Besengu alitoa kauli ya kupinga waziwazi, akisema pamoja na baadhi ya Makadinali wengine, hakutakuwa na baraka kwa wapenzi wa jinsia moja barani Afrika.

Robert Sarah – Guinea

dc

CHANZO CHA PICHA, LE CARDINAL ROBERT SARAH

Maelezo ya picha, Kardinali Robert Sarah kutoka Guinea

Kardinali Robert Sarah kutoka Guinea ana vigezo vya kuchaguliwa kuwa Papa. Yeye ni mhafidhina katika kanisa.

Aliteuliwa akiwa na umri wa miaka 34 kama Askofu wa Conakry, mwanatheolojia huyo mwenye umri wa miaka 79 alikumbwa na utata Januari 2020 kwa kitabu cha, “From the Depths of Our Hearts,” alichodai kimeandikwa na Sarah na Papa Benedict XVI.

Tatizo lilikuwa Papa Benedict XVI hakukubali kwamba aliandika kitabu hicho, na jina lake likaondolewa wakati wa uchapishaji.

Peter Kodwo Appiah Turkson – Ghana

f

CHANZO CHA PICHA, CNA

Maelezo ya picha, Kardinali Peter Turkson wa Ghana katika mkutano na waandishi wa habari Oktoba 23, 2015.

Kadinali Peter Turkson ,76, Askofu mkuu wa Cape Coast nchini Ghana, pia anakidhi kuwa Papa. Aliteuliwa kuwa Kardinali na Papa John Paul II mwaka 2003.

Turkson ni Chansela wa Chuo cha Upapa na Sayansi ya Jamii. Alitetea uamuzi wa Francis wa kubariki watu wa mapenzi ya jinsia moja, tofauti na makasisi wengi barani Afrika, na hataki mapenzi ya jinsia moja yaharamishwe.

Hilo likamweka katika msuguano na Maaskofu wa Ghana na taasisi za kisiasa za Ghana ambapo ni haramu kujitambulisha kama mtu wa LGBTQ. Turkson pia amekuwa mstari wa mbele kuzungumzia mabadiliko ya tabia nchi na mazingira.

Anthea Butler, Profesa wa masomo ya dini na masomo ya Africa katika Chuo Kikuu cha Pennsylvania, Marekani, anasema, “chochote kinaweza kutokea, lakini, usifikirie chochote.”

Ufitinema Aime Gerard

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *