Yafahamu matunda hatari zaidi duniani

Matunda ni ovari zilizokomaa, zilizoiva za mimea ya maua ambayo humiliki mbegu na mara nyingi ni chakula kitamu.
Ni sehemu muhimu ya mzunguko wa uzazi wa mmea, kusaidia kutawanya mbegu na kuwezesha ukuaji wake.
Lakini mara nyengine matunda sio tu kuhusu ladha ya juisi yake na faida zake za kiafya.
Wakati mwingine, nyuma ya mwonekano wao wa kuvutia, harufu ya kupendeza zipo hatari kwa afya ya binadamu.
1. Manchineel – Tufaa la Kifo

CHANZO CHA PICHA, THINKSTOCK
Tunda hili linalojulikana kama “tufaha la pwani” au “tufaha la kifo,” huficha tishio lake kuu nyuma ya mwonekano wake .
Matunda ya mti huu huvutia, huwa na harufu nzuri , yana ladha kama matufaha ya kawaida. Lakini, mguso mmoja wa tunda hili unaweza kusababisha matatizo ya kupumua.
Sehemu hatari zaidi ya tunda hili ni utomvu wake.
Tone ndogo la utomvu huo wenye sumu ya phorbol na hippomane, linaweza kuchoma ngozi yako na kukusababishia maumivu makali.
Kutoka kugusa hadi kula, mwingiliano wowote na sehemu za mti huu unaweza kusababisha madhara makubwa, kuanzia matatizo ya tumbo kutetemeka mwili mzima kwa ghafla, na hata kifo.
Ikipatikana sehemu za Carebean, katika taifa la Mexico, Amerika ya Kusini, na sehemu za Florida Kusini, Manchineel umetajwa kuwa mti hatari zaidi duniani.
Kulingana na jarida la East Fruit, Utomvu wake umetumiwa na watu wa kiasili kama silaha, na rekodi za kihistoria zinaonyesha kuwa ni sumu hii iliyomuua mvumbuzi Juan Ponce de León mwaka 1521.
Hata wakati wa mvua, ni hatari kusimama chini ya mti wa Manchineel kujikinga mvua kwani matone ya maji yanayotoka katika matawi yake yanaweza kusababisha malengelenge kwa mwili wa binadamu.
Utomvu huo una kutu kiasi kwamba unaweza hata kuharibu rangi ya gari.
Inaonekana kwamba hekaya ya “matofaa ya ufuoni” si hadithi tu bali ni onyo zito kwa wale wanaokaribia sana mti huo wenye hila.
2. Matunda ya Ackee (Blighia sapida) – Mchanganyiko wa Hatari

CHANZO CHA PICHA, GETTY IMAGES
Matunda yake ni madogo na yenye mvuto wa hali ya juu na kwa muda mrefu yamekuwa ishara ya vyakula vya Jamaika.
Matunda haya ya kigeni, yanayothaminiwa na wapenzi wengi wa chakula, hutumiwa katika maandalizi ya sahani za jadi.
Hatahivyo, mwonekano wa tunda hili sio kama lilivyo. Kwa upande mmoja, tunda la ackee linapoiva, ni salama kutumia na kwa upande mwengine iwapo halijaiva linabeba sumu kwa jina hypoglycin A, ambayo inaweza kusababisha hali inayojulikana kama “ugonjwa wa kutapika wa Jamaika.”
Dalili za ugonjwa huu zinaweza kujumuisha kutapika, hypoglycemia, katika hali mahututi na hadi kifo.
Mchakato wa kukomaa wa ackee pia unavutia kabisa.
Matunda ambayo yako tayari kuliwa hufunguka, na kufunua nyama yao ya manjano iliyoiva.
Ishara hii ya asili inaonyesha kwamba sumu haipo tena na matunda ni salama kula.
Licha ya hatari zake, Wajamaika hupata nyama iliyoiva ya ackee kuwa chanzo chakula kizuri.
Tunda hili la juisi na lenye lishe ni sehemu muhimu ya vyakula vya kitaifa vya Jamaika.
Mojawapo ya sahani maarufu za kitamaduni zilizo na ackee ni “ackee na saltfish.”
Katika sahani hii, cod ya chumvi inakamilishwa na nyama ya maridadi ya ackee, na kujenga mchanganyiko maalum wa ladha ya kipekee.
Wajamaika wanaheshimu tunda hili na wanajua kwa hakika wakati bora wa kulivuna na kulitayarisha.
Kwao, ackee sio tu tunda lakini sehemu muhimu ya urithi wa kitamaduni na utambulisho wa kitaifa.
Ackee ni mfano wazi wa jinsi asili inavyoweza kuchanganya hatari na faida, ikihimiza kuunda upishi bora ambao una shangaza na kufurahisha.
3. Cherry

CHANZO CHA PICHA, PA MEDIA
Unakumbuka jinsi wakati mwingine unaishia kutafuna au kumeza mbegu ya tunda kwa bahati mbaya? Naam, jaribu kuepuka hilo unapokula tunda la cherries.
Matunda haya madogo yanayong’aa na yenye ladha hubeba mbegu ambazo zinaweza kukuua.
Ndiyo, kulingana na utafiti uliochapishwa kwenye ResearchGate, mbegu ndani ya tunda la cheri zina sumu inayoitwa sianidi hidrojeni.
Ingawa mbegu moja au mbili ukimeza kwa bahati mbaya haziwezi kukudhuru, ikiwa utameza kwa kiasi kikubwa inaweza kusababisha kifafa, mshtuko wa moyo na hata kusababisha kifo.
4. Matunda ya Nyota

CHANZO CHA PICHA, ISTOCK
Matunda ya nyota hupatikana kote duniani.
Matunda haya ni matamu na yanafanana na umbo la nyota baada ya kulikata na hupendwa na watu wengi.
Lakini nyuma ya mwonekano huo wa nyota , tunda hilo lina sumu iliojificha
Kulingana na utafiti uliochapishwa kwenye tovuti ya Taasisi ya Kitaifa ya Afya (NIH), tunda la nyota au carambola lina kiasi kikubwa cha oxalates ambazo zinaweza kuunganishwa na kalsiamu kuunda mawe ya figo na kusababisha uharibifu wa figo.
Matunda haya ni hatari sana kwa watu ambao tayari wana matatizo ya figo
5. Jatropha

CHANZO CHA PICHA, ISTOCK
Jatropha ni mmea ambao unaweza kupatikana katika hali ya hewa ya kitropiki kote duniani.
Mbegu katika matunda haya matamu ya rangi ya majanno yanayong’aa huwa na kiwango kikubwa zaidi cha sumu inayoitwa ricin ambayo inaweza kusababisha kutapika, kuhara, maumivu ya tumbo na hisia inayowasha kwenye koo.
Nchini, India, kumekuwa na visa vingi vya watoto kupata sumu ya tunda hili.
Utafiti uliochapishwa katika Jarida la Kimataifa la Utafiti wa Matibabu na Mapitio ulichambua data kutoka mwaka wa 2004 hadi 2013 na kugundua jumla ya kesi 169 za sumu kali ya Jatropha kwa watoto.