Ndoa tano za wasanii wakubwa duniani zilizofungwa kimya kimya

Linapokuja suala watu maarufu katika tasnia ya muziki, mashabiki wao hutegemea kuona shughuli kubwa za wasanii hao zikiwa hadharani na pengine zikisimamisha shughuli za nchi. Kama ndoa ya hivi karibuni ya msanii kutoka Tanzania, Juma Jux, na mwanadada kutoka Nigeria, Priscilla Ojo.
Lakini hali ni tofauti kwa baadhi yao, wengine huchagua ndoa za siri. Hakuna kamera wala mwaliko wa watu wengi. Ndiposa swali linaibuka; kwa nini huamua kufanya ndoa za siri?
Zipo sababu kadhaa, moja ni kuzingatia ubora wa harusi na si wingi wa watu. Vilevile, wengine hutaka kuepuka kuchunguzwa na kamera za vyombo vya habari na macho ya umma.
Kuwa na orodha ndogo ya wageni, wanandoa hupata wasaa mzuri wa kujumuika vizuri na wageni wote. Hupata fursa ya kumuona kila mtu na kuwa na karibu na kila mgeni, na kuzingatia sherehe yao bila ya hofu ya fedheha au jambo la aibu.
Harusi za faragha hazina shinikizo kubwa, kwani hakuna muda wa kuzingatia matarajio ya wengine, ili kukidhi masilahi ya mashabiki. Na hilo huzifanya harusi hizi kuwa na gharama ndogo pia.
Zijue baadhi ya ndoa za faragha za wasanii wakubwa duniani:
Diamond & Zuchu

CHANZO CHA PICHA, MITANDAO
Siku ya jana, Msanii Naseeb Abdul ama Diamond Platnumz kutoka Tanzania na mpenzi wake Zuhura Othman, Zuchu, walitangaza kufunga ndoa. Lakini ujumbe wa Diamond juu ya ndoa hiyo, unaonekana kuwachanganya wengi huku wengine wakisema, wawili hao tayari wameachana. Lakini madai hayo yanakinzana na ujumbe wa mama mzazi wa Diamond, Mama Dangote ambaye kupitia Instagram yake, amethibitisha ndoa hiyo.
Licha ya ndoa hii kuwa ya siri, watu mbalimbali mitandaoni wamejitokeza kuwapa hongera wawili hawa na wengine bado wakiwa na wasiwasi. Zuchu akiwa na Diamond amepachika video Snapchat akiwa na mumewe kuonesha kuwa mambo ni moto.
Jay Z & Beyoncé

CHANZO CHA PICHA, GETTY IMAGES
Wasanii wa Marekani, Beyoncé na Jay-Z walifunga ndoa kwa siri Aprili 4, 2008, huko Manhattan, Marekani. Licha ya kufanya harusi kuwa siri na kutotangaza mipango ya harusi hiyo, pia wana ndoa hao hawakutangaza uchumba wao.
Harusi ilifanyika katika jumba la kifahari la Jay-Z huko Manhattan, New York. Wageni waliohudhuria waliombwa waache nyumbani simu zao za BlackBerry ili kutunza ufaragha wa tukio hilo.
Justin Bieber & Hailey Baldwin

CHANZO CHA PICHA, BUSSINESINSIDER
Msanii Justin Bieber na Hailey Baldwin walifanya harusi ya siri huko New York City, Septemba 2018. Ndoa hiyo ilifanyika miezi miwili baada ya kuchumbiana huko Bahamas, Julai 7, 2018, kwa mujibu wa mtandao wa People.
Ndoa yao ya faragha mahakamani, ilifuatiwa na sherehe kubwa huko South Carolina Septemba 2019. Sherehe ya kwanza ilikuwa ndogo, wakati sherehe ya pili ilihudhuriwa na wageni 154, wakiwemo wana familia na marafiki.
Cardi B & Offset

CHANZO CHA PICHA, JEFF KRAVITZ/FILMMAGIC
Msanii Cardi na Offset walioana kwa siri Septemba 20, 2017, kabla ya rapa huyo wa kundi la Migos kumchumbia kwenye jukwaa kwenye tamasha la Power 99 la Powerhouse huko Philadelphia Oktoba mwaka huo huo.
Kulingana na Hakimu wa Kaunti ya Fulton huko Georgia, Cardi aliwasilisha kesi ya talaka dhidi ya Offset miaka mitatu baadaye, Septemba 15, 2020. Na ndoa hiyo ikasambaratika.
Ed Sheeran & Cherry

CHANZO CHA PICHA, RTE
Msanii Ed Sheeran alifunga ndoa na mchumba wake wa tangu utotoni, Cherry Seaborn, katika sherehe ndogo ya siri Desemba 2018. Harusi hiyo ilikuwa ya siri na marafiki wachache wa karibu na familia ndio walikuwepo. Ed na Cherry baadaye walifanya sherehe kubwa na marafiki na familia zao.
Ed Sheeran, raia wa Uingereza, alizungumza juu ya harusi hiyo ya siri katika mahojiano, akifichua kwamba walichagua kuiweka siri ili kuepusha vyombo vya habari na mapaparazzi.
Nicki Minaj & Kenneth

CHANZO CHA PICHA, INSTAGRAM
Msanii Nicki Minaj – ambaye alichumbiana na Kenneth Petty chini ya mwaka mmoja kabla ya ndoa – alithibitisha Oktoba 2019, juu ya ndoa yake katika video kwenye Instagram ambayo inaonyesha vikombe vya kahawa vya Bwana na Bibi na kofia za bibi na bwana harusi.
Akizungumza kwenye kipindi chake cha Queen Radio, Nicki alisema: ‘Lazima niifanyie kazi albamu yangu na nina mengi ya kuzingatia na ndio maana sitaki kufanya harusi kubwa sasa. Tutafanya harusi kubwa baadaye.