Rwanda inatarajia kuwa mwenyeji wa mkutano wa kimataifa utakaojadili mikakati ya kutokomeza Virusi ya UKIMWI
Katika mkutano huu wa kila mwaka utakaoendelea kwa muda wa siku tano kuanzia tarehe 14 hadi 17 Julai 2025, washiriki watajadili hatua zinazopigwa katika upatikanaji wa tiba ya kisasa kwa watu waliokwisha ambukizwa virusi vya UKIMWI, pamoja na masuala mengine muhimu.

Bi JERO Plimo, ambaye ni kiongozi wa shirika linaloongozwa na vijana ‘Youth-led organization’ na pia ni mwakilishi wa ‘Reproductive Health Program’ (IRO Kenya), alizungumzia mambo muhimu yatakayojadiliwa katika mkutano huu na matarajio yao kama vijana.
“Baadhi ya mambo tutakayojadili ni juhudi za kuhakikisha kwamba serikali zetu zinakuwa na mchango wao wa moja kwa moja, kwa kuwa kwa muda mrefu tumekuwa tukitegemea misaada kutoka kwa mataifa ya nje. Kwa maoni yangu, ni muhimu sasa kufikiria jinsi nchi zetu za Afrika zinaweza kuzisukuma serikali zetu kutenga bajeti mahsusi kwa ajili ya kusaidia mipango ya kupambana na UKIMWI, kifua kikuu na malaria. Jambo lingine ni kutafakari kuhusu miradi inayoanzishwa na kuendeshwa na wananchi wenyewe, hususan walengwa wa hizo programu, ili kujaza pengo tunaloliona kwa sasa.”
Serikali ya Marekani ilikuwa ikitoa mamilioni ya dola kupitia Mpango wa Dharura wa Rais wa Marekani kwa ajili ya Kukabiliana na UKIMWI barani Afrika ‘PEPFAR’ (President’s Emmergency Plan for AIDS Relief Africa) , ambao ulifadhili shughuli mbalimbali zinazohusiana na UKIMWI kama vile huduma za afya, elimu, utafiti, na kuwawezesha watu wanaoishi na virusi vya UKIMWI kupitia miradi ya maendeleo binafsi, na mengineyo. Hata hivyo, kwa sasa kumekuwa na pengo kubwa kutokana na kufungwa kwa baadhi ya njia za ufadhili kulikosababishwa na uamuzi wa serikali yao. Hapa ndipo Bi. Florence Riako Anam, kiongozi wa GNP+, anapotoa wito kwa serikali za mataifa husika kuchukua hatua za haraka ili kuziba pengo hilo.

Alisema kwamba: “Katika mabadiliko ya kitu yoyote huleta misukosuko, huleta woga , huleta shauku, mambo kama hayo ndio watu wanapitia saa hii lakini jikumu letu ni kushawishi watu wafanye kazi na bushaishi serikali ijumuwike na watu wao ili tujalibu kuangalia vile tutakavowenda mbele, maana yake yote kabisa watu wanawishi na Virus sisi tunaomba, tuendelee kuishi, hatutaki kufa!”
Katika mkutano huu wa kimataifa, inatarajiwa kwamba Rwanda itaoneshwa kama nchi iliyopiga hatua kubwa katika kufikia malengo yaliyowekwa na Shirika la Afya Duniani (WHO), ambayo ni: asilimia 95 ya watu wanaoishi na virusi vya UKIMWI wawe wanajua hali yao, asilimia 95 kati yao wawe wanatumia dawa za kupunguza makali ya virusi, na asilimia 95 ya wale walioko kwenye tiba wawe wamepunguza maambukizi mapya.

Katibu Mtendaji wa Umoja wa Watu Wanaoishi na Virusi vya UKIMWI nchini Rwanda, Dkt. MUTAMBUKA Deo (PhD), amesema kuwa kwa kuwa mkutano huu unafanyika wakati ambapo misaada ya kimataifa iliyokuwa inasaidia watu wanaoishi na virusi imekatizwa, kuna haja ya juhudi kutoka kwa serikali pamoja na ushirikiano wa kutosha kati ya walengwa ili kuziba pengo hilo.
Amesema: “Kujitegemea ni safari! Ukirudi nyuma ukaangalia tulikotoka kama taifa na jinsi misaada ya kigeni imekuwa ikikatizwa, naona kuwa kwa sasa tunayo bahati kuwa na serikali inayoweka raia mbele ya yote. Kwa hiyo, sidhani kama kama taifa tumeshangazwa na hali hii kwa sababu tunaiona ikija, lakini tunajua kuwa uongozi wetu upo kuhakikisha ulinzi wa wananchi na kutafuta suluhisho kwa pamoja. Pale ambapo dawa zinapatikana, na tunaposhirikiana na Wizara ya Afya pamoja na RBC, huwa wanatueleza kuwa dawa zipo na ni zile muhimu kabisa.”
Akaongeza: “Jambo la pili ni kupunguza maambukizi mapya. Haya yote ni majukumu yetu kama umoja wa watu wanaoishi na virusi vya UKIMWI hapa nchini, lakini pia ni jukumu la serikali. Sasa tunatakiwa kufanya kazi kwa pamoja badala ya kila mmoja kufanya kivyake. Nadhani huo ndio ufunguo wa kupatikana kwa suluhisho lenye mafanikio.”

Katika mwaka uliopita wa 2024, zaidi ya watu 630,000 duniani walifariki kutokana na magonjwa yanayohusiana na UKIMWI. Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), Dkt. Tedros Adhanom Ghebreyesus, alisisitiza kuwa kila mtu ana haki ya kupata huduma bora za afya.
Alisema: “Tambua haki yako ya kupokea huduma bora za afya, elimu na taarifa zinazokuhusu. Kila mtu ana haki ya kupata huduma muhimu za afya anazohitaji, wakati wowote na popote alipo, kwa gharama anazoweza kumudu. Viongozi wenu wawajibishwe kwa maamuzi yao, na wananchi waelimishwe na wahamasishwe kushiriki kikamilifu katika mambo yanayowahusu pamoja na kufuatilia utekelezaji wake, kwa sababu haki ya afya imo mikononi mwako.”
Takwimu kutoka Shirika la Afya Duniani zinaonesha kuwa kufikia mwaka 2024, kulikuwepo kati ya watu milioni 37 hadi milioni 45 waliokuwa wanaishi na virusi vya UKIMWI duniani kote. Katika mwaka huo huo, watu wapya takribani milioni 1.3 waliambukizwa virusi hivyo, ambapo asilimia 45 ya waathirika hao walikuwa wanawake na wasichana wa rika mbalimbali.
