Rais wa Madagascar asema ‘nimejificha mahali salama’ huku akionya kuhusu jaribio la mapinduzi

Rais wa Madagascar asema ‘nimejificha mahali salama’ huku akionya kuhusu jaribio la mapinduzi

Rais wa Madagascar Andry Rajoelina amesema “nimejificha mahali salama” baada ya jaribio la kumuua, kufuatia wiki kadhaa za maandamano ya kumtaka ajiuzulu.

Katika matangazo ya moja kwa moja kwa taifa kupitia ukurasa wa Facebook, Rajoelina, 51, alisema “kundi la wanajeshi na wanasiasa walipanga kuniua”.

Hakufichua eneo aliko, lakini ripoti ambazo hazijathibitishwa awali zilidokeza kwamba alitoroka nchini kwa ndege ya kijeshi ya Ufaransa.

Hilo limetokea baada ya maandamano ya nchi nzima, hasa yakiongozwa na vijana, yenye lengo la kumuondoa madarakani.

Jaribio lililofeli la Rajoelina kuwatuliza waandamanaji hao vijana – walioitwa “Gen Z Mada” – lilimshuhudia rais akiifuta kazi serikali yake yote na kufanya makubaliano mengine bila mafanikio.

Hajaonekana tangu Jumatano, na mwishoni mwa wiki ofisi ya Rajoelina ilisema jaribio lilikuwa linaendelea kumlazimisha kuondoka madarakani.

Hotuba yake kwa taifa ilicheleweshwa mara kadhaa Jumatatu huku kukiwa na machafuko, wanajeshi nao wakitishia kuteka makao makuu ya Televisheni ya taifa katika kisiwa cha Bahari ya Hindi.

Hatimaye, katika matangazo ya Facebook alisema: “Tangu Septemba 25, kumekuwa na majaribio ya kuniua na ya kufanya mapinduzi. Kundi la wanajeshi na wanasiasa walipanga kuniua.

“Nililazimika kutafuta mahali salama ili kulinda maisha yangu.”

“Kuna njia moja tu ya kutatua masuala haya; ambayo ni kuheshimu katiba inayotumika nchini”.

Ufitinema Aime Gerard

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *