Je, teknolojia ya utoaji mikopo itabadilisha sura ya huduma ndogo za kifedha nchini Rwanda?
Ni katika muktadha huo ambapo siku ya Jumanne ilizinduliwa rasmi taasisi ya kifedha inayotumia teknolojia, NUMIDA, ambayo inatarajiwa kurahisisha upatikanaji wa mikopo na kuwafikia watu ambao kwa kawaida hawafikiwi na taasisi za kifedha za jadi.
NUMIDA inakuja wakati wafanyabiashara wengi wadogo bado wanakumbana na changamoto mbalimbali, zikiwemo masharti magumu, viwango vya juu vya riba, pamoja na muda mrefu unaohitajika ili kupata mikopo kutoka benki za kawaida.

NISHIMWE Teddy, mfanyabiashara anayefanya kazi katika jiji la Kigali, eneo la Cartier Commercial, ni miongoni mwa walionufaika na huduma hii. Anasema mabadiliko ni makubwa ikilinganishwa na hali aliyokuwa amezoea hapo awali.
“Hapo zamani nilihitajika kuwa na dhamana na nyaraka nyingi. Sasa naomba mkopo kupitia simu, na ndani ya saa chache ninaupata. Hii imenisaidia kuongeza bidhaa katika biashara yangu.”
Hata hivyo, licha ya kupongezwa kwa mfumo huu mpya, wataalamu wanaonya kuwa kasi ya utoaji mikopo inaweza pia kuleta hatari, ikiwemo kuchukua mikopo inayozidi uwezo wa kuirejesha, hasa kwa wale wasio na uelewa wa kutosha kuhusu usimamizi wa fedha.
Meneja wa mikopo katika NUMIDA, Rurangwa Joyce, anasisitiza kuwa wameweka mifumo ya kupunguza hatari hizo.
“Tunatumia taarifa za biashara za mteja pamoja na teknolojia kutathmini uwezo wake kabla ya kumpa mkopo. Hii inatusaidia kutoa mikopo inayolingana na uwezo wake.”
Kwa upande wa BNR, inaelezwa kuwa kuongezeka kwa taasisi kama hizi kunaweza kuwa na mchango mkubwa katika kukuza uchumi wa taifa, hasa kwa kuwafikia watu ambao kwa muda mrefu hawakuwa wakipata huduma za kifedha.

Mkurugenzi anayesimamia taasisi zisizo za benki katika BNR, James Gasana, anasema taasisi hizi zinaweza kusaidia kwa kiasi kikubwa wanawake na vijana.
“Kwa kawaida makundi haya hayapati mikopo kutokana na ukosefu wa dhamana. Teknolojia hii inaweza kubadilisha hali hiyo na kuwawezesha kuwekeza katika miradi yenye faida.”
Hata hivyo, bado kuna changamoto ya ukosefu wa elimu ya matumizi sahihi ya mikopo, jambo ambalo linaweza kusababisha baadhi ya watu kuingia kwenye madeni makubwa.
Hii inaonesha kuwa pamoja na kurahisisha upatikanaji wa mikopo, kuna haja ya kuongeza elimu kwa wananchi kuhusu usimamizi wa fedha.

Mkurugenzi Mtendaji wa NUMIDA, Minah Shahida, anasema lengo lao si kutoa mikopo pekee.
“Tunataka kuwasaidia wajasiriamali wadogo kukua na kuendeleza biashara zao; si kuwapa fedha tu, bali kuwasaidia pia kuzitumia kwa ufanisi.”
Tangu NUMIDA ianze shughuli zake nchini Rwanda mwezi Machi mwaka huu, tayari imetoa mikopo yenye thamani ya zaidi ya faranga za Rwanda milioni 120 kwa watu 150, jambo linaloonesha uwepo wa uhitaji mkubwa sokoni.
NUMIDA ina uzoefu wa takriban miaka 10 katika ukanda wa Afrika Mashariki, ikifanya kazi katika nchi kama Kenya, Uganda na Tanzania.
Picha:






