RDDP II Yabadilisha Maisha ya Ngendahayo: Kutoka kwa Ng’ombe Aliyetoa Lita Moja ya Maziwa hadi Kuingiza Milioni Mbili za Faranga za Rwanda

 

Wakati ufugaji wa ng’ombe unaendelea kuwa moja ya nguzo muhimu za maendeleo vijijini nchini Rwanda, wananchi wengi wanaendelea kunufaika na Mradi wa Maendeleo ya Sekta ya Maziwa Awamu ya Pili (RDDP II).

Ismael Ngendahayo, mkazi wa Kijiji cha Akabuga, Sekta ya Kiramuruzi katika Wilaya ya Gatsibo, ni miongoni mwa wanaoshuhudia jinsi mradi huu ulivyobadilisha maisha yake kutoka kwenye ufugaji usio na tija hadi kuwa mfugaji mwenye mafanikio na mzalishaji wa malisho bora yanayouzwa kwa wafugaji wengine.

Ngendahayo anasema kuwa kabla ya kufikiwa na RDDP II, alikuwa akifuga ng’ombe waliotoa maziwa kidogo kutokana na ukosefu wa maarifa kuhusu lishe bora ya mifugo pamoja na upatikanaji mdogo wa malisho yenye ubora.

Alianza kulima malisho bora katika eneo dogo la mita 20 kwa 20. Hata hivyo, baada ya kuona matokeo chanya, aliendelea kupanua eneo hilo hadi kufikia hekta mbili.

Kwa sasa analima aina mbalimbali za malisho bora, ikiwemo Chloris gayana, Brachiaria, Panicum, Napier 1112, Mucuna na Desmodium, ambayo husaidia kuongeza uzalishaji wa maziwa na kuboresha afya ya mifugo.

Ngendahayo anaeleza kuwa hapo awali alikuwa akilima aina moja tu ya malisho kutokana na ukosefu wa maarifa. Kupitia mafunzo aliyopata kutoka RDDP II, alielewa umuhimu wa lishe kamili kwa ng’ombe ili kuongeza uzalishaji.

Anasema:

“Ng’ombe ni kama binadamu. Anahitaji chakula cha kujenga mwili na chakula cha kumpa nguvu. Nilianza na eneo dogo, lakini baada ya kutumia malisho bora, nikaona tatizo la njaa kwa mifugo likipungua na uzalishaji wa maziwa ukiongezeka kwa kiasi kikubwa.”

Mabadiliko hayo yameonekana wazi. Wakati hapo awali ng’ombe wake alikuwa akitoa kati ya lita moja hadi moja na nusu kwa siku, sasa anatoa zaidi ya lita kumi kwa siku.

Ngendahayo anaongeza kuwa mafunzo aliyopata yalimwezesha kuelewa jinsi ya kuandaa lishe kamili ya mifugo, ambapo asilimia 75 ya chakula ni cha kutoa nguvu na asilimia 25 ni cha kujenga mwili.

“Leo ng’ombe wangu anatoa zaidi ya lita kumi za maziwa kwa siku. Tulifundishwa jinsi ya kuchanganya vizuri vyakula vya mifugo ili kupata lishe bora inayoongeza uzalishaji wa maziwa”. anasema.

Mbali na kuongezeka kwa uzalishaji wa maziwa, kilimo cha malisho bora pia kimemletea faida kubwa kiuchumi. Katika mavuno yake ya hivi karibuni, baada ya kutosheleza mahitaji ya mifugo yake, aliingiza zaidi ya faranga za Rwanda milioni mbili.

Pia huuza mbegu za malisho kwa bei ya faranga 5,000 za Rwanda kwa kilo moja na ameajiri wafanyakazi wa kudumu kumi.

Ngendahayo anaishukuru RDDP II kwa kumpatia si tu mbegu za malisho bali pia maarifa yaliyomwezesha kuboresha ufugaji wake.

“RDDP II haikunipatia mbegu pekee, bali pia maarifa ya kutunza ng’ombe, kujenga banda bora na kudumisha usafi kama ninavyotunza nyumba yangu mwenyewe,” anasema.

Kwa siku zijazo, analenga kupanua zaidi mashamba ya malisho bora, kujenga ghala la kuhifadhi malisho na kupata mashine za kisasa za kukausha na kufungasha malisho ili yaweze kupatikana mwaka mzima.

Anaamini hatua hiyo itawawezesha wafugaji wasiokuwa na uwezo wa kulima malisho yao wenyewe kupata malisho bora kwa urahisi na hivyo kuongeza uzalishaji wa maziwa nchini.

Safari ya Ismael Ngendahayo inaonyesha jinsi uwekezaji katika malisho bora pamoja na maarifa sahihi ya ufugaji unavyoweza kubadilisha maisha ya mfugaji na kuongeza uzalishaji wa maziwa. Kupitia RDDP II, changamoto zilizokuwa zikikabili wafugaji wengi zinaendelea kubadilishwa kuwa fursa za maendeleo endelevu na ustawi wa jamii za vijijini nchini Rwanda.

Picha: 

Kupitia RDDP II, Ngendahayo ameshuhudia mafanikio makubwa katika maisha na shughuli zake za ufugaji.

Ngendahayo akieleza furaha yake kutokana na ongezeko la uzalishaji wa maziwa kutoka kwa ng’ombe wake.

 

 

Ufitinema Aime Gerard

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *