Expo Rwanda 2026 Kuanza Julai 28, Kuwaleta Waonyeshaji Zaidi ya 500

Expo Rwanda 2026 Kuanza Julai 28, Kuwaleta Waonyeshaji Zaidi ya 500

Maonesho ya Kimataifa ya Biashara Rwanda 2026 Kuanza Julai 28, Yakitarajiwa Kuwaleta Zaidi ya Waonyeshaji 500.

Kigali, 3 Julai 2026 , Shirikisho la Sekta Binafsi nchini Rwanda (PSF), kwa ushirikiano na Wizara ya Biashara na Viwanda (MINICOM), limetangaza rasmi kurejea kwa Maonesho ya 29 ya Kimataifa ya Biashara ya Rwanda (Rwanda International Trade Fair – Expo 2026), yatakayofanyika kuanzia tarehe 28 Julai hadi 17 Agosti 2026 katika Viwanja vya Maonesho vya Gikondo, jijini Kigali.

Maonesho hayo, ambayo ni makubwa na yenye hadhi ya juu zaidi nchini Rwanda, yanatarajiwa kuwaleta pamoja wafanyabiashara, wawekezaji, wajasiriamali, wazalishaji, watoa huduma na watumiaji kutoka Rwanda na mataifa mbalimbali duniani. Lengo ni kuonyesha bidhaa na huduma, kuwasilisha ubunifu, kutangaza fursa za uwekezaji, pamoja na kuimarisha ushirikiano wa kibiashara kupitia mikutano ya biashara kati ya kampuni (B2B).

Kwa mujibu wa waandaaji, toleo la mwaka huu linatarajiwa kushirikisha zaidi ya waonyeshaji 500 wa ndani na wa kimataifa, huku zaidi ya wageni 300,000 wakitarajiwa kutembelea maonesho hayo katika kipindi cha siku 21. Aidha, washiriki kutoka zaidi ya nchi 20 wanatarajiwa kushiriki, jambo linaloendelea kuimarisha nafasi ya Expo ya Rwanda kama jukwaa muhimu la biashara, uwekezaji na ushirikiano wa kikanda.

Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa PSF, Bw. Callixte Kanamugire, amesema kuwa Expo 2026 si maonesho ya kawaida bali ni jukwaa la kimkakati linalochochea ukuaji wa biashara, ubunifu, uwekezaji na ushirikiano wa kikanda.

“Maonesho ya Kimataifa ya Biashara ya Rwanda 2026 ni zaidi ya maonesho ya bidhaa; ni jukwaa muhimu la kukuza biashara, ubunifu, uwekezaji na ushirikiano wa kikanda. Tunazialika kampuni za ndani na za kimataifa, washirika wa maendeleo, taasisi za serikali pamoja na wananchi wote kushiriki kuanzia tarehe 28 Julai hadi 17 Agosti 2026 katika Viwanja vya Gikondo. Kwa pamoja tuonyeshe ubora wa Rwanda na dunia, tujenge ushirikiano mpya na kufungua fursa zitakazochangia ukuaji endelevu wa uchumi na ustawi wa jamii.”

Waandaaji wameeleza kuwa Expo 2026 itawapa waonyeshaji fursa ya kupanua masoko yao, kuanzisha ushirikiano wa kimkakati wa kibiashara, kuzindua bidhaa mpya na kukutana na maelfu ya wateja pamoja na wawekezaji watarajiwa.

PSF pia imewahimiza wafanyabiashara, taasisi za serikali, washirika wa maendeleo na wananchi kwa ujumla kushiriki katika tukio hilo muhimu litakaloonesha uwezo wa biashara za ndani, kikanda na kimataifa.

Usajili wa waonyeshaji tayari umefunguliwa, huku kampuni zinazotaka kushiriki zikihimizwa kujisajili mapema ili kuhakikisha zinapata nafasi ya kuonesha bidhaa na huduma zao katika maonesho hayo.

Ufitinema Aime Gerard

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *