Gatsibo Yaimarisha Sekta ya Maziwa Kupitia Mradi wa RDDP II


Mradi wa Awamu ya Pili wa Maendeleo ya Sekta ya Maziwa nchini Rwanda (RDDP II) unaendelea kuleta mageuzi makubwa katika ufugaji wa ng’ombe wa maziwa wilayani Gatsibo, huku uzalishaji wa maziwa ukiongezeka kutokana na upatikanaji bora wa maji, mifugo yenye tija na mafunzo kwa wafugaji.

Mradi huo unaotekelezwa kwa ushirikiano kati ya Serikali ya Rwanda na Mfuko wa Kimataifa wa Maendeleo ya Kilimo (IFAD), kupitia Wizara ya Kilimo na Mifugo (MINAGRI) pamoja na Bodi ya Kilimo na Rasilimali za Wanyama Rwanda (RAB), unalenga kuendeleza ufugaji wa kisasa na kuongeza kipato cha wafugaji.

Makamu wa Meya wa Wilaya ya Gatsibo anayeshughulikia Maendeleo ya Uchumi, Sekanyange Jean Leonard, amesema kuwa mradi huo tayari umeonyesha matokeo chanya kwa jamii.

“Tumeshagawa zaidi ya ng’ombe 150 wa maziwa wenye tija kubwa na kuwapa mafunzo maafisa ugani 56 wanaowasaidia wafugaji kutumia mbinu za kisasa za ufugaji. Lengo letu si kumiliki mifugo pekee, bali kuongeza uzalishaji wa maziwa kwa matumizi ya kaya na biashara,” alisema.

Kwa mujibu wa wafugaji, maboresho ya miundombinu ya maji yamekuwa miongoni mwa mambo yaliyochangia mafanikio hayo.

Muyambi Peter, mkazi wa kijiji cha Nyamatete katika Sekta ya Rwimbogo, anasema zamani mifugo yao ililazimika kutembea umbali mrefu kutafuta maji, jambo lililosababisha uchovu, magonjwa na uzalishaji mdogo wa maziwa.

“Hapo awali ng’ombe walitembea zaidi ya kilomita tano kutafuta maji. Walichoka na kutoa maziwa machache sana. Sasa wanatoa kati ya lita 10 hadi 15 kwa siku, jambo ambalo limeongeza mapato yetu,” alisema.

Miongoni mwa miradi muhimu inayotekelezwa ni ukarabati na upanuzi wa bwawa la Rwiminazi, ambalo linatarajiwa kuongeza upatikanaji wa maji kwa wafugaji na wakazi wa eneo hilo.

Msimamizi wa mradi huo, Bizimana Jean De Dieu, alisema uwezo wa bwawa hilo unaongezwa kutoka mita za ujazo 31,000 hadi 49,000, huku kazi zikitarajiwa kukamilika mapema mwezi Julai.

Aliongeza kuwa miundombinu mipya itazuia mifugo kuingia moja kwa moja kwenye bwawa na kuchafua maji, huku sehemu maalum za kuchotea maji zikijengwa kwa ajili ya wafugaji na wananchi.

Bwawa hilo linahudumia zaidi ya ng’ombe 20,000 na pia kutoa maji kwa matumizi ya nyumbani na shughuli mbalimbali za kiuchumi.

Kutokana na maboresho hayo, ukusanyaji wa maziwa wilayani Gatsibo umeongezeka kutoka lita 45,000 kwa siku miaka miwili iliyopita hadi lita 60,000 kwa sasa. Wilaya hiyo inalenga kufikia uzalishaji wa lita 100,000 za maziwa kwa siku katika miaka ijayo.

Kupitia RDDP II, Gatsibo inaendelea kubadilika kutoka ufugaji wa jadi kwenda ufugaji wa kisasa unaozingatia tija, ambapo maji ya uhakika, mifugo bora na maarifa ya wafugaji vinatajwa kuwa msingi wa maendeleo endelevu katika sekta ya maziwa.

 

 

Ufitinema Aime Gerard

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *